Salamu – Julai, 2022

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ni furaha yetu moyoni kukualika tena kwenye kona hii ya salamu za mwezi. Mimi na familia yangu tu wazima.

Naamini hata wewe Mungu amekupa uzima. Naamini pia Mungu amekupa ulinzi na afya na uhai. Kwetu mwezi wa sita tumekuwa na semina huko Tunduma, tumekuwa na semina Vwawa huko mkoa wa Songwe, na tumekuwa na semina ya Vijana wa kanisa la Uinjilisti wa Tanzania nzima.

Tunamshukuru Mungu kwa kutupatia nafasi hiyo ya kumtumikia.

Hebu tuanze kuziangalia salamu za mwezi huu. Kumbuka tunasalamu zenye kichwa “WEKA BIDII YA KUUSHUGHULIKIA MOYO AU NAFSI YAKO”

Katika salamu zilizopita tulianza kuangalia jambo la tatu linaloweza kupelekea jeraha moyoni nalo lilikua ni kuwa na mtu muhimu kwako.

Katika salamu za mwezi huu nataka tusogee mbele kidogo tuangalie jambo la nne.

4: JAMBO LA NNE NALO NI HILI; KUTARAJIA KITU KISICHO KUWA

Moja ya umivu au jambo linaloweza kusababisha jeraha moyoni mwa mtu ni hili la kutarajia jambo ambalo linaweza kuwa limechelewa au lisiloweza kutokea kabisaa.

Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima. (Mithali 13:12)”

Kwa mujibu wa mistari hiyo unajifunza kuwa nafsi ya mtu anayesubiria kitu kinachoweza kuchelewa anaweza kukutana na hatari ya kupata jeraha moyoni litakalopelekea kuugua. Ngoja nikupe mifano hii michache.

Watu wengi ambao leo hii wanatarajia kupata mtoto, na mtoto huyo akakawia kuja, mioyo ya watarajia hao wengi hujikuta kwenye majeraha mengi mnoo.

Wengi huugua moyoni na matokeo ya kuugua kwao huko moyoni hutokea mpaka huku nje.

Wengi hujikuta wakiwa ni watu waliokosa kujiamini, chuki, hasira nk. Wengi hujikuta wana magonjwa mengi sana.

Angalia mfano wa mwanamke huyu aitwae Hana. “Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwani huli chakula? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi? Ndipo Hana akainuka, walipokwisha kula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la BWANA. Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana… Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za BWANA. Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa.” (1Samweli 1:8-10 na 15-16)

Ukimtazama Hana alikua na jeraha moyoni lililosababishwa na kukawia kwake kupata mtoto.. Watu wengi wanaopitia katika jambo kama hili, wengi mioyo yao imejeruhika sana.

Mfano mwingine ni huu wa kutarajia mtu furani kubadilika tabia, watu wengi hasa Wakristo wamejikuta wakiwa na majeraha moyoni kisa ni hiki cha kutarajia kuona mabadiliko ya tabia kwa mtu fulani na mabadiliko hayo yakakawia kuja.

Wengi huomba, hufundisha n.k., wanapoona mabadiliko hayo hayatokei huugua moyoni. Na kujikuta katika maumivu mengi.

Sikiliza, unaweza leo hi ukawa ni mtu uliyekosa furaha kabisa kisa ni hiki cha kukawia tu kuolewa. Wafuatilie mabinti wengi sana ambao wanatarajia kuolewa na jambo hilo likakawia wengi hujikuta wakiwa na uchungu moyoni.

Mfano mwingine ni huu, Watu wengi wanapokea ahadi mbalimbali kutoka kwa Mungu. Na kwa bahati mbaya wengi hujijengea moyoni matarajio ya kuzipokea hizo ahadi haraka mnoo.

Ukiwa ni mtu wa sifa hii, nakuhakikishia utakua na uchungu moyoni kisa unaona kama Mungu kakudanganya nk. Mungu hasemi uongo

Ngoja nikupe mfano huu wa Yeremia. Angalia mistari hii. “Ole wangu, mama yangu, kwa kuwa umenizaa mtu wa kuteta, na mtu wa kushindana na dunia yote! Mimi sikukopesha kwa riba, wala watu hawakunikopesha kwa riba; lakini kila mmoja wao hunilaani. BWANA akasema, Hakika nitakutia nguvu upate mema; hakika nitamlazimisha adui akusihi wakati wa uovu, na wakati wa taabu……” “Ee BWANA, unajua wewe; unikumbuke, unijilie, ukanilipie kisasi juu yao wanaoniudhi; usiniondoe kwa uvumilivu wako; ujue ya kuwa ni kwa ajili yako nilivyopatikana na mashutumu.Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee BWANA, Mungu wa majeshi.Sikuketi katika mkutano wao wanaojifurahisha, wala sikufurahi, naliketi peke yangu kwa sababu ya mkono wako; kwa maana umenijaza ghadhabu. Mbona maumivu yangu ni ya daima, na jeraha yangu haina dawa, inakataa kuponywa? Je! Yamkini wewe utakuwa kwangu kama kijito kidanganyacho, na kama maji yasiyodumu?Kwa sababu hiyo BWANA asema hivi, Ukirudi, ndipo mimi nitakapokurejeza, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia wewe, bali hutawarudia wao.Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema BWANA.Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha.” (Yeremia 15:10-11 na 15-21)

Kwa mujibu wa mistari hiyo unaona namna Yeremia alivyojikuta katika maumivu makubwa yasiponyeka moyoni mwake kisa ni hiki hiki cha kutarajia kwa haraka kukutana na ahadi zile Mungu kamuahidi.

Mungu alimuahidi mambo mengi mno. Moja ya hizo ahadi ni hizi. “BWANA akasema, Hakika nitakutia nguvu upate mema; hakika nitamlazimisha adui akusihi wakati wa uovu, na wakati wa taabu…”

Mungu alimpa hizo ahadi, bahati mbaya ukiangalia utagundua ahadi hizo zilichelewa. Yeremia alipoona ahadi hizo hazipati akawaza kama alidanganwa hivi; Mungu alimwambia wazi kuwa shida ipo kwake yeye Yeremia.

Ahadi ya Mungu ilibaki vile vile, Mungu alimwambia kuwa anatakiwa arudi na akae vizuri ili amwokoe dhidi ya hao wanaomjeruhi Yeremia.

Sikiliza, jifunze kutokua na matarajio ya kupata kitu kwa muda uutakao wewe… msubiri Mungu.

Biblia inasema hivi. “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu……” (2Petro 3:9).

Mungu hakawii kukupa hicho alichokuahidi kukupa, ondoa haraka ya kukipata ndipo utakua mzima huko moyoni mwako.

Naamini umeona jambo hili namna linavyoweza kuwa chanzo cha jeraha moyoni.

Tuonane tena katika kona hii mwezi ujao. Naamini umenielewa sana.Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

 1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
 2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
 3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
 4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
 5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
 6. DVDs au CDs
 7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
 8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
  • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
  • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
  • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
 9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako

Mwl. Steven na Beth Mwakatwila

Leave a Reply

Your email address will not be published.