Salamu – Novemba, 2011

Bwana Yesu asifiwe sana mpendwa. Tunamshukuru Mungu aliyetuwezesha kupata uzima na afya njema, Ni imani yetu kuwa pia hata wewe Bwana amekutunza na kukupa amani. Mwezi uliopita tumekuwa na mambo mengi sana, tumekuwa na semina nyingi pia na safari ndefu kutoka kwetu Mbeya mpaka Dar es Salaam, ambako tulikuwa na semina nzuri sana ya ndoa na vijana. Tulipewa na Bwana somo lenye kichwa cha ‘Mambo muhimu unayotakiwa uyafanye ili upate kuilinda na kuiponya ndoa yako.’ Kwa kweli tumeona jinsi shetani alivyozijeruhi ndoa nyingi sana, na pia tulimwona Bwana Yesu akiziponya na kuzilinda hizo ndoa. Kwa vijana tulikuwa na somo lenye kichwa ‘Mambo muhimu unayotakiwa uyafanye kabla ya kuoa na kuolewa.’ Mwezi huu tupo Mbeya tutafunga hema letu kwenye viwanja vya chekechea mjini Mbalizi. Tuombeeni, tuna tarajia kuwa na wiki zuri mbalizi. Tukimaliza tuataelekea Kahama, Bwana akipenda. Hebu tuingie kwenye salamu za mwezi huu. Kumbuka tuna salamu zenye kichwa:-  

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UMUOMBE MUNGU KILA SIKU. (ENEO LA KUYAJUA MAPENZI YAKE AU MAKUSUDIO YA MUNGU)

“Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.” (1Yohana 5:14-15) 

Ukiyasoma maneno hayo utagundua ya kuwa Mungu yupo tayari kutupa sisi kitu chochote kile tumuombacho. Lakini ili atupe ametupa agizo kuwa lazima tuombe sawasawa na mapenzi yake ndipo tutakapo pewa kila tumuombacho. Neno mapenzi ya Mungu maana yake ni kusudi au mipango ya Mungu. Kwa maana nzuri ili Mungu atupe kile tunachokihitaji ni lazima tufahamu kwanza ni nini makusudi ya Mungu katika hilo tunaloliomba, hapo ndipo tutakapopewa hicho tumuombacho 

Katika salamu zilizopita tuliendelea kuangalia katika lile eneo la njia azitumiazo Bwana Mungu kusema na mtu, tuliendelea kwenye ile njia ya pili ya ndoto na maono. Na tuliangalia lile eneo la maombi maalumu ili Mungu akutengenezee macho yako ya ndani yapewe nuru, pia uombe ili akupe roho ya ufunuo. Mwezi huu tuone tena kitu kingine, nacho ni:-  

MUOMBE ROHO MTAKATIFU AKUFUMBULIE FUMBO USILOLIELEWA LILOKUJA KATIKA NDOTO AU MAONO 

Ili uanze kuona au kujua ni nini maana ya njozi uliyopokea ambayo imekuja kwako kama fumbo unatakiwa uanze leo hii kufanya maombi ya mara kwa mara:-

Kumuomba Roho Mtakatifu akuwezeshe wewe kupata ufahamu wa hicho ulicho kiona na hujakielewa yaani kimekuja kwako kama fumbo, ili ufasiriwe maana yake ni nini, lazima umuombe Roho Mtakatifu ambaye ni yeye peke yake ayajuaye mafumbo ya Mungu. Neno la Mungu linasema hivi:- 

“Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila ni roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi TUPATE KUYAJUA TULIYOKIRIMIWA NA MUNGU” (1Kor 2:10-12) 

Nimeyaandika maneno hayo kwa herufi kubwa ili niweke msisitizo hapo, ili wewe na mimi tuyajue tuliyokirimiwa na Mungu, aliamua kutupa Roho Mtakatifu ambaye ndiye mwenye jukumu la kutujulisha ni nini maana ya kila alichotupa Mungu, kiwe ni neno nk. Mungu anapozungumza nasi kwa njia ya ndoto hata maono inawezekana akasema halafu wewe usielewe kabisa. Watu wengi husema nimeona hivi au nimeota hivi au nimesikia hivi lakini sijaelewa! Mtafute Roho Mtakatifu yeye anajua kila fumbo ambalo limetoka kwa Mungu. Mungu anasema kwenye kitabu cha Yeremia:- 

“Niite nami nitakuitikia, nami ntakuonyesha mambo makubwa magumu usiyoyajua” (Yeremia 33:3) 

Ukienda kumuomba Mungu yeye anasema ukimwita akufahamishe ni nini yaliyo mapenzi yake, au hata kama hujamuomba ila yeye ameamua kukufahamisha jambo, anaweza kukuonesha au kusema na wewe jambo ambalo kwako linaweza kuwa gumu yaani usilolielewa kabisa! Sasa akisema na wewe neno kama hilo kwa sauti au kwa maono au kwa ndoto, inatakiwa umuombe Roho mtakatifu akufasirie hilo fumbo. Mungu aliposema na Farao, alimwonyesha Ng’ombe na masuke saba, unajua bila Mungu mwenyewe kufasiri maana yake ni nini hakuna mtu angelijua. Yusufu alifahamu kuwa Mungu peke yake ndiye ayajuaye yaliyomo moyoni mwake ni nini, kumbuka Roho Mtakatifu ni Mungu. Yusufu alimwambia Farao maneno haya:- 

“Yusufu akamjibu Farao, akisema, si mimi: Mungu atampa Farao majibu ya amani.” (Mwanzo 40:16) 

Yusufu alijua kuwa Mungu pekee ndiye mwenye uwezo wa kujua alichokifumba. Hata kwako leo hii Mungu akikuonyesha fumbo, fahamu anayelijua hilo fumbo ni yeye mwenyewe, rudi kwake, muombe akufumbulie hilo fumbo. Kumbuka Roho mtakatifu peke yake ndiye anayejua mafumbo ya Mungu kwa kuwa Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe. Sasa kinacho wapa watu wengi taabu ni hiki; wengi wakiona, wanakimbilia kwa watu fulani wakifikiri watu hao ndio wanaojua kufasiri ndoto, sikia hawajui! Anayejua ni Roho Mtakatifu, kama wameifasiri basi si wao, ni Roho Mtakatifu aliye ifasiri. Ninachotakakukwambia ni hiki, kama Mungu amesema na wewe anaweza kukufasiria wewe pia! Mtumishi mwenzangu usichukue utukufu wa Mungu kwa kujiona kuwa wewe unajua kufasiri, wewe hujui kitu, ila Mungu Roho Mtakatifu ndiye anaye kuwezesha kwa hiyo usijivune hata kidogo. Yusufu alimwambia wazi Farao kuwa si yeye ila Mungu ndiye atayemfasiria. 

Ukimuomba Mungu akupe uwezo wa kufasiri ndoto au maono atakupa kabisa. Ona; aliwapa hawa ndugu zetu uwezo huo 

“Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote na ndoto.” (Danieli 1:17) 

Danieli alipewa na Mungu uwezo wa kufahamu habari za ndoto na maono yote, yaani kufasiri, kujua chanzo cha ndoto au ono ni nini, nk. Mungu hata leo anataka sana sisi tuwe na mawasiliano naye, tuelewe amesema nini; iwe kwa njia ya maono au ndoto. akisema nawe kwa njia ya ndoto au ono au kwa fumbo, inatakiwa umuombe akupe uwezo wa kufahamu ni nini maana ya hilo fumbo. OMBA AKUPE WEWE UWEZO HUO! Swali langu kwako ni hili, kwa nini Mungu aseme na wewe halafu wewe usijue ila ajue mwingine, huoni kama wewe ndio mwenye tatizo? 

Swali nitajuaje sasa maana? Ukimwomba Mungu akufasirie hicho ulichokiona na hukifahamu maana yake, fahamu anaweza kukufasiria kwa kukuonyesha ono lingine ambalo ndani yake ameweka ufahamu wa wewe kuelewa amesema nini, kasha utaelewa amesema nini. Hebu tuone mfano huu, alipozungumza na Farao, aliirudia ile ndoto mara mbili, mara ya kwanza alimuoyesha ng’ombe, mara ya pili alimuonyesha masuke. Yusufu alielewa kuwa ndoto aliyoiona Farao ni ndoto moja. Mungu aliposema na Farao kwa mara ya kwanza, Farao hakuelewa, akasema naye mara ya pili, pia hakuelewa. Ona neno la Mungu linasema hivi.  

“Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, usingizi mzito uwajiapo watu katika usingizi kitandani; ndipo huyafunua masikio yao.” (Ayubu 33:14-16) 

Mungu anaweza kurudia nakurudia tena kukuletea ono au ndoto ile ile mpaka uelewe. Anachotafuta ni kukuona wewe ukimwomba akufasirie pale ambapo hujamuelewa. Usiogope kumwambia wazi kuwa ‘sijaelewa, naomba nieleweshe’. Sisi tusipoelewa tunaiacha hiyo ndoto au hilo ono. Hata akisema kwa sauti yake neno ambalo ni fumbo, hatutafuti kuomba kufasiriwa hilo fumbo. Hata kwa kunena kwa lugha, neno linasema anenaye kwa lugha aombe kufasiri, ili aelewe ni nini alichokuwa anaomba au kumuadhimisha Mungu 

“Kwa sababu hiyo yeye anenaye kwa lugha na aombe apewe kufasiri.” (1Kor 14:14) 

Ngoja nikupe mfano huu namna Mungu alivyokuwa akimfasiria Danieli maono au ndoto. Alikuwa anamletea fasiri kwa kupitia ndoto au maono akilala 

“Ndipo Danieli akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Hanania, na Mishaeli, na Azaria wenzake; ili wombe rehema kwa Mungu wa mbinguni kwa habari ya siri hiyo,ili kwamba Danieli na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli. Ndipo Danieli alipofunuliwa siri hiyo katika njozi ya usiku…… Yeye hufunua mambo ya fumbo na ya siri;…. Basi, Danieli akaenda kwa Arioko, aliyewekwa na mfalme kuwaangamiza wenye hekima wa Babeli; alikwenda akamwambia hivi; Usiwaangamize wenye hekima wa Babeli; Niingize mimi mbele ya mfalme, nami nitamwonyesha mfalme ile tafsiri” (Danieli 2:17-24) 

Ukiyasoma maeno hayo utagundua hiki ninacho kuambia, Mungu alimfunulia Danieli fasiri ya ile ndoto ya mfalme kwa kutumia ndoto ya usiku, si usiku tu, hata mchana anaweza kusema na wewe, Mungu anaweza kukufunulia fasiri ya maono au ndoto kwa kutumia ndoto au ono atakayo kuonyesha tena. Ngoja nikupe mfano huu; Siku moja nilipokuwa kiongozi wa timu ya maombi ya sehemu niliyokuwa naishi, niliona picha au ono mara mbili, dada mmoja ninaye mfahamu, nikajiuliza swali kwa nini namuona huyo dada? Mchana alinijia dada mmoja akaniambia hivi, Steven, unajua dada fulani anaroga huduma ya maombi? Akamtaja yule dada ambaye mara mbili nimemuona kwenye maono usiku.  

Nikamwambia anarogaje? Akasema wewe si mtumishi wa Mungu, kamuulize Mungu atakuambia. Kweli siku ile nikapata shida sana, kwani usiku mara mbili Bwana amenionyesha sura ya huyo dada, halafu mchana naambiwa hivyo. Nikaondoka kwenda nyumbani kwangu, ilikuwa jioni kama saa kumi na moja hivi. Nilipokuwa naomba Mungu anifasirie ni nini maana ya maono yale ya usiku, na kutaka kujua huo urogaji wa huyo dada. Unajua? Ghafla, nguvu za Mungu zilinishukia mle chumbani, nikaaanza kunena kwa nguvu ya ajabu sana, macho yangu yakapata nguvu za ajabu, nikaona mle chumbani yule dada amesimama mbele yangu akiwa mtupu kabisa. Huku naendelea kuomba nikamuona wazi wazi huyo dada mbele yangu. Nikasikia sauti ya Bwana ikasema; Steven, huyo dada ni mzinzi, na amewasababishia hata baadhi ya kina dada wengine wawili waingie kwenye tabia ya uzinzi. Unajua alinifasiria maana ya maono yale kwa njia hiyo. Nikakaa na hao kina dada wawili kilammoja peke yake wakakubali kuwa kweli wamefanya uzinzi, na kila mmja akaniambia kuwa dada huyo ndiye aliyewapeleka sehemu fulani bila kujua kumbe wamepangana huko wanaume watatu ambao huyo dada aliwafahamu, aliwaomba wamsindikize, kumbe kawatega. Wakalala huko na kuzini. Sikia; hata wewe ukiweka bidii ya kuomba Roho Mtakatifu akufasirie atakufasiria tu. Ninaamini umenielewa, hebu anza kuomba leo, utaona mabadiliko katika eneo hilo. Mungu akubariki sana na tuonane tena mwezi ujao. 

Wako 

Mr. Steven & Mrs. Beth Mwakatwila 

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetuer adipiscing elit, sed diam nonummy nibh euismod tincidunt ut laoreet dolore magna aliquam erat volutpat.