Bwana Yesu Kristo asifiwe! Tunamshukuru Mungu kwa kutupa mwezi huu wa nane.
Ninawashukuru sana watu wote kwa kutuombea katika mwezi uliopita. Tumekuwa na huduma nzuri, na tulizimaliza salama huko Ubaruku, Chimala, na Arusha.
Ninawaletea salamu za mwezi huu wa nane. Kumbuka tuna salamu zenye kichwa:
JIFUNZE KUTAKA KARAMA AU KUOMBA MUNGU AKUPE KARAMA YA MIUJIZA NA UPONYAJI (SEHEMU YA PILI)
Hebu tusogee mbele kidogo.
6: MUUJIZA, MOJA YA MALENGO YAKE NI KUMPA MUNGU SHUKRANI AU KUMTUKUZA MUNGU
Moja ya sababu zinazoweza kumfanya Mungu afanye miujiza ni kuwa na lengo la kutufundisha ili tumshukuru Mungu.
Sikia, unaposikia neno kumshukuru Mungu, ndani yake kumebeba pia kumtukuza Mungu. Biblia inasema hivi:
"Atoaye dhabihu za kushukuru ndiye anayenitukuza; naye autengenezaye mwenendo wake nitamwonyesha wokovu wa Mungu." (Zaburi 50:23)
Ukiisoma mistari hiyo, utajifunza kwa upana kuhusu habari za kumshukuru Mungu. Sikia, unapomshukuru Mungu ndipo unapomtukuza Mungu.
Sasa sikia, kila mtoto wa Mungu anatakiwa amtukuze Mungu au amshukuru Mungu. Ndani ya muujiza unaotoka kwa Mungu umebeba tabia ya watu kumshukuru Mungu.
Sikia, unapotendewa muujiza wowote kutoka kwa Mungu, unajikuta unaanza kumtukuza au kumshukuru Mungu.
Angalia mistari hii uone ninachokuambia:
"Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika. Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wako wapi? Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu?" (Luka 17:12–18)
Ukiisoma mistari hiyo, utaona kuwa Bwana Yesu Kristo alitenda muujiza ambao ndani yake kulikuwa na nguvu ya uponyaji. Angalia jambo hili: ndani ya ule muujiza kulikuwa na nguvu ya kuwafanya waliotendewa muujiza wamtukuze, wampe utukufu, au wamshukuru Mungu.
Bwana Yesu Kristo alisikitika sana alipowaona wale watu tisa hawakurudi kumshukuru Mungu baada ya kuwatendea muujiza. Kitendo cha Bwana Yesu Kristo kusikitika kwa sababu ya watu hao kutokurudi kumpa Mungu utukufu kinatufundisha kuwa tunapokutana na miujiza tuliyotendewa na Mungu, tuwe na tabia ya kushukuru au kutoa ushuhuda wa mambo aliyotutendea Mungu.
Angalia mistari hii:
"Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia BWANA wimbo huu, wakanena, na kusema, Nitamwimbia BWANA, kwa maana ametukuka sana; farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. BWANA ni nguvu zangu, na wimbo wangu; naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu; ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza. BWANA ni mtu wa vita, BWANA ndilo jina lake. Magari ya Farao na jeshi lake ameyatupa baharini; maakida yake wateule wamezama katika Bahari ya Shamu." (Kutoka 15:1–4)
Sikia, baada ya muujiza mkubwa alioufanya Mungu siku ile alipoigawa Bahari ya Shamu na kuwaangamiza wanajeshi wote wa Farao, kila mtu aliyeona na hata anayesimuliwa jambo hilo alimshukuru au kumtukuza Mungu. Siku ile hadi leo, muujiza huo unaendelea kumpatia Mungu utukufu.
Sikia, moja ya sababu inayomfanya Mungu kufanya miujiza ni ili watu wamrudishie Mungu utukufu au shukrani. Sikia, kanisa linalokosa miujiza fahamu kuwa linapoteza nafasi ya Mungu kutukuzwa.
Unapotafuta Mungu akutendee muujiza au unapoona miujiza, fahamu unatengenezewa tabia ya kumshukuru Mungu kila unapotendewa muujiza au unapotoa ushuhuda wa mambo makuu aliyokutendea Mungu.
Unajua watu wengi wana msemo wa kuwaambia watu wasitafute miujiza. Sikia, unapowaambia watu wasitafute miujiza katika maisha yao, iwe mtu mmoja mmoja, kundi, au taifa, wanapoteza tabia ya kumshukuru Mungu. Sikia, mtu akitendewa muujiza na Mungu hujikuta akimshukuru Mungu.
Si yeye tu aliyetendewa muujiza, hata wale wanaoshuhudia au kuuona huo muujiza alivyofanyiwa mtu, nao humshukuru Mungu.
Unajua, mimi nikitazama mfumo wa maisha ninayoishi sasa, na hata ninapofikiria habari za mbinguni, ninaona ni muujiza tu wa Mungu. Kula kwangu, kupata kazi, kupewa mke na watoto, na hata leo kumtumikia Mungu, kwa kweli maisha yangu ni muujiza kutoka kwa Mungu.
Kuna wakati nikikaa na kuangalia maisha yangu, elimu yangu, na nilivyokuwa, naona kuwa kama si muujiza wa Mungu kwangu, nisingekuwa hivi. Hata uhai na uzima nilionao naona ni miujiza ya Mungu. Namshukuru sana Bwana Yesu Kristo.
Kwa hiyo, naomba kila siku Mungu anitendee miujiza au atende miujiza kupitia mimi ili Mungu atukuzwe sana.
Naona sasa umeanza kujifunza kuomba Mungu akupe karama ya miujiza. Karama hii ya miujiza na uponyaji ni pana mno. Mungu anaweza kukutunza wewe kimiujiza, na mengine mengi.
Angalia mfano huu mwingine:
"Ukaniite siku ya mateso; nitakuokoa, na wewe utanitukuza." (Zaburi 50:15)
Angalia, Mungu anaweza kuwaokoa watu na kuwatoa kwenye mateso kwa kutumia muujiza au jambo ambalo si la kawaida kwa mwanadamu. Mfano, ulikuwa na ugonjwa akakuponya kiajabu.
Ukikutana na muujiza huo wa uponyaji, Mungu anataka kila aliyetendewa hivyo amshukuru au amtukuze Mungu.
Naamini umenielewa.
Tuonane katika salamu za mwezi ujao.
Ukihitaji masomo yetu, unaweza kuyapata kwa njia zifuatazo:
1. App yetu ya huduma yenye jina “HUSONEMU (MWAKATWILA)” — inapatikana Play Store, ambapo kuna masomo mengi sana.
2. Tovuti yetu: www.mwakatwila.org
3. YouTube: HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU
4. Facebook: ingia kwenye tovuti yetu uone alama ya Facebook (f), kisha “like” ili upate maelezo ya kujiunga, au tafuta “SOMA NENO LA MUNGU”
5. Instagram: tafuta “Huduma ya Soma Neno la Mungu”
6. DVDs 📀 au CDs 💿
7. Vitabu
NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733 ili kupata vitabu, DVD na CD.
8. Kwa njia ya redio:
- Rungwe FM 102.5 MHz — Jumapili saa 3:00 hadi 4:00 usiku
- Baraka FM 107.7 MHz — Jumanne saa 12:00 jioni hadi 1:00 usiku
- Bomba FM 104.1 MHz — Ijumaa saa 3:00 hadi 4:00 usiku
9. Online Radio: radio.mwakatwila.org
Ratiba ya vipindi:
- Saa 12:00 asubuhi
- Saa 07:00 mchana
- Saa 12:00 jioni
- Saa 03:00 usiku
10. Ingia MWAKATWILA YouTube Online
Kwa mawasiliano zaidi:
+255 754 849 924
+255 756 715 222
Wako,
Mwl. Steven Mwakatwila & Beth Mwakatwila